[Documents menu] Documents menu

From: ds@VOA.GOV (Dave Simonds)
To: Multiple recipients of list <swahili-l@relay.doit.wisc.edu>
Subject: Tanzania Election 95

Tanzania Election 95

By Emmanuel Muganda, Voice of America, 29 August 1995

MUHIMU: Maoni, majibu, maswali, malalamiko, n.k., yote
tafadhalini yatume kwa SWAHILI-L au TANZANET au
EMMANUEL_MUGANDA@AFR.VOA.GOV.

Ndugu zangu wote katika net hii,
Makala ifuatayo nimeipata muda mfupi tu kutoka gazeti la RAI toleo la Juni 8-14. Nimeona afadhali niwanakilishie.

URAIS NA HATIMA YA TAIFA

Makala hii imeandikwa na Dk. Rugatiri D.K. Mekacha, Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam.

Mojawapo ya mambo ambayo nchi hii itayarithi kutoka kwa uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi ni kushuka kwa viwango vya utendaji na ufanisi wa ofisi hiyo iliyo kuu kuliko zote katika nchi. Kwa kuwa Ali Hassan Mwinyi ameweza kila mtu anajiona kuwa ataweza.

Enzi za Rais Julius K. Nyerere si wengi walidhani wanaweza. Maana wengi wa hao wanaojitokeza sasa walikuwapo tangu enzi hizo na hawakuthubutu kujitokeza. Kujitokeza kugombea ni kuimarika kwa democrasia. Watu watapata fursa pana zaidi ya kuchagua mtu, siyo kwa sababu wengine hawapo bali kwa sababu miongoni mwa waliojitokeza watamwona anafaa.

Lakini hao wanaojitokeza wamejipima kwa vigezo gani hata wakaona wanafaa kuwa marais wa nchi hii? Maana tunaambiwa wamo hata wale ambao walishiriki katika kuvunja katiba waliyoapishwa kuilinda. Wamo hata walioshindwa katika nyadhifa nyingine hata ikabidi waondolewe au walazimishwe kujiuzulu. Wamo pia hata wale ambao imethibitika kuwa wamechangia katika kulipotezea taifa mapato ya kodi. Baada ya hayo yote sasa wanataka urais!

Ni kweli kuwa mfumo uliokuwapo ulikuwa wa "mizengwe" kama anavyokiri Mwalimu mwenyewe. Lakini ni lazima pia tukiri kuwa viwango vya utendaji wa ofisi hiyo vilikuwa vya juu mno kulinganisha na majukumu yaliyoikabili.

Majukumu hayo ni kama vile kupigania uhuru, kujenga taifa kutokana na mkusanyiko wa makabila, kulipa "identity" na mwelekeo taifa hilo, kujenga na kudumisha amani na utulivu, kupambana na ukoloni mamboleo na ujinga, kuleta haki na usawa, kushiriki katika kuendeleza ukombozi wa Afrika, kupambana katika vita baridi na kadhalika.

Labda athari nyingine ya utawala wa rais Mwinyi ni kwa Mwalimu Nyerere mwenyewe. Kushusha viwango vya sifa za urais wa Tanzania. Kwa maana ya kuwa Mwalimu anamwona rais ajaye kama mziba nyufa na wala siyo mjenzi wa nyumba.

ANATETEA MASLAHI YA NANI?

Ni kweli kuwa 'nyumba' yetu haiwezi kuendelea kujengwa kabla nyufa zilizojitokeza hazijazibwa. Lakini kazi ya kuziba nyufa ni kazi ndogo sana katika jumla ya majukumu ya rais. Kwa hiyo, kwa maoni yangu, kuziba nyufa alizozitaja Mwalimu ni sifa za msingi tu za kiongozi au hata mrasimu wa ngazi yoyote katika nchi.

Nadhani rais wa nchi iwayo yoyote lazima awe na zaidi ya sifa za "mshona viraka." Lazima aweze kusanifu na kushona mavazi wanayoyataka wateja wake. Yaani, lazima aweze kubainisha walimpigia kura, abainishe matakwa yao na abuni siasa na mikakati ya kutekeleza siasa hiyo. Kisha aitekeleze siasa hiyo kwa ari na uwezo wake wote.

Alipokuwa Rais, Mwalimu Nyerere alibainisha constituency yake ya kuwa wakulima na wafanyikazi. Siasa zake zililenga katika kuwanufaisha hao. Walau ndivyo alivyosema. Yawezekana matokeo ya utekelezaji wa siasa hiyo hayakuwanufaisha walengwa kwa namna alivyokusudia. Lakini hakuna ushahidi kuwa alikusudia kutenda kinyume cha hivyo alivyosema.

Nimesoma maoni ya kila mgombea aliyehojiwa katika RAI. Hakuna hata mgombea mmoja ambaye ameeleza anataka kutetea matakwa ya nani. Yawezekana kuhoji kuwa hawataji watawakilisha matakwa ya nani kama mbinu ya kisiasa ya kutotaka kuwabagua baadhi ya watu wanaowatarajia wawapigie kura.

Lakini kueleza wanasimamia matakwa ya nani ni jambo la msingi sana kwa sababu tatu. Sababu ya kwanza ni kuwa kauli kama hiyo itatusaidia kulinganisha maneno na matendo yao ya siku za nyuma na ya sasa. Kwani tunaambiwa wapo wanaoungwa mkono na mataifa makubwa ya nje. Tunaambiwa pia kuwa wapo wanaofanya kampeni kwa kutumia mapesa ya Waajemi (Iran.)

Tunaambiwa wapo wanaofanya kampeni kwa mapesa ya mabepari wenye asili ya Kiasia wa humu humu nchini. Tunaambiwa wapo wanaofanya kampeni kwa mapesa ya mabepari "wazawa." Tunaambiwa wapo wanaofanya kampeni kwa mapesa ya mabepari wenye asili ya Kiasia kutoka Kenya. Je, matakwa ya hao wanaotoa mapesa hayo ni sawa na matakwa ya wakulima wa Serengeti?

Sababu ya pili ni kuwa baada ya miaka mitano, au hata kabla, tutahitaji vigezo vya kutusaidia kuwahukumu hao tutakaokuwa tumewachagua. Je, matakwa watakayokuwa wameyawakilisha ni hayo hayo waliyosema watayawakilisha? Ikibidi yafaa watu wapate fursa ya kumuondoa madarakani kwa taratibu nzuri za kidemokrasia kiongozi atakayethibitika kuwa amekwenda kinyume na matakwa yao.

Kitendo cha kukataa kusema wanataka kuwakilisha matakwa ya nani ni sawa na kukataa kujiwekea malengo, au hawana kabisa malengo? Ni sawa na kusema na kukataa kujiwekea vigezo vya kujipima. Ni sawa na kusema kuwa watang'ang'ania madaraka hata ikithibitika kuwa hawafai, kama ilivyoonekana katika uongozi unaomaliza muda wake. Ni sawa na kukaribisha uwezekano wa wao kuondolewa madarakani kwa njia zisizo za kidemokrasia.

Sababu ya tatu inatokana na hali ya kisiasa nchini. Katika kipindi cha uongozi wa rais Mwinyi, hasa katika miaka mitano ya mwisho, matakwa ya mabepari wa kimataifa yalizingatiwa mno hata pale ambapo yaliathiri matakwa ya wananchi kwa nchi hii. Siyo siri kuwa ubinafsishaji, kadri unavyotekelezwa sasa, umewanyang'anya wananchi mali yao na kuikabidhi mikononi mwa wageni.

Siyo siri kuwa pale wanaponufaika wananchi imekuwa siyo katika umoja wao bali mmoja mmoja. Wengi wa hao mmoja mmoja wamekuwa ni wale ambao ni wachuuzi na siyo wazalishaji. Tena wengi wa hao walionufaika wamekuwa ni wenye asili ya Kiasia. Kwa hiyo sambamba na matakwa ya mabepari wa nje, yamezingatiwa sana matakwa ya kundi moja la mabepari wa ndani.

Siyo siri kuwa siasa ya "soko huria" kadri inavyotekelezwa sasa imeligeuza taifa kuwa jaa la kina aina ya bidhaa hata zile zilizooza na zenye madhara ya kiafya kwa watumiaji. Hili limesababisha uzalishaji wa humu nchini kufa kabisa. Lakini yapasa tujiulize: Hao wanaotuuzia bidhaa zao tunawalipa na nini? Tutaendelea kuwalipa na nini? Hao wanaotaka kuwa viongozi wetu wanalo jibu?

Matokeo ya ubinafishaji wa soko huria ni ukosefu wa ajira, kupunguzwa kwa maendeleo ya vijijini kulikozua "umachinga," kulitumbukiza taifa na watu wake katika umaskini uliokithiri, na kuzua itikadi na dhana za kibaguzi kama "wazawa" na "magabacholi" zinazoweza kuliangamiza taifa.

Binafsi siamini hayo ndiyo matakwa ya wananchi wa nchi hii. Kutobainisha ni matakwa ya nani wagombea wetu wanataka kuyasimamia ni sawa na kusema kuwa mambo kadri yalivyo sasa ndiyo murua na kwamba wataendelea kusimamia matakwa yanayosimamiwa na uongozi wa sasa. Hii ni kusema kuwa wanadhamiria kuendelea kuliangamiza taifa.

Kutokana na urithi wa democrasia ya chama kimoja na itikadi ya CCM yawezekana baadhi ya hao wagombea wakahoji kuwa watasimamia matakwa ya kitaifa. Hii itakuwa ni kudanganya kwa sababu mbili. Sababu ya kwanza ni kuwa hakuna matakwa ya kitaifa. Kila tabaka lina matakwa yake. Na tutake tusitake viongozi huwakilisha matakwa ya tabaka hili au lile.

Matakwa ya mkulima wa pamba hayawezi kuwa sawa na matakwa ya mchuuzi wa pamba. Hili linajulikana wazi. Wakulima wa wilaya ya Serengeti kwa mfano, wanajua kuwa wachuuzi wa pamba ambao sasa wamejivisha ngozi ya kondoo na kujiita wakombozi wa wakulima hawawakilishi matakwa yao. Kwa kujua hivyo wachuuzi hao sasa wanatumia itikadi ya ukabila kujihalalisha.

Sababu ya pili ni kuwa siasa haiendeshwi kwa makubaliano. Serikali ni mkondo mmoja tu wa dola ambayo jukumu lake ni kusimamia matakwa ya tabaka moja dhidi ya matakwa ya matabaka mengine. Hii ndiyo sababu tunadai kujua wanaogombea urais na hata ubunge wanawakilisha matakwa ya nani.

NI ITIKADI AU USOKWE MTU?

Nadhani hata leo ukimwuliza Mwalimu Nyerere atakuambia kuwa yeyeni mjamaa. Sio wengi watakaokataa. Watakaoafiki watafanya hivyo siyo kwa sababu yeye hujiita hivyo. Bali ni kwa sababu ya kauli pamoja na matendo yake. Historia imempiga mhuri huo.

Lakini siasa ya ujamaa haikunyesha kama mvua. Wala Mwalimu hakuipata katika ndoto. Mwalimu siyo ujamaa na ujamaa siyo Mwalimu. Ujamaa ni siasa iliyoibuka na kuhalalishwa na mazingira maalumu ya kisiasa. Kwa kifupi mazingira hayo yalikuwa yale ya taifa lililokuwa linaibuka kutoka katika ukoloni na ambalo lilikuwa linahangaika kutafuta mwelekeo na identity yake isiyofungamana na ubepari wala ukomunisti.

Karl Marx alipata kuulizwa kama yeye ni mfuasi wa itikadi ya Ki-Marx. Akajibu akasema:"Nashukuru Mungu Siyo." Asingeweza kuwa mfuasi wa siasa ya ki-marx kwa kuwa yeye ndiye Marx. La ajabu ni kuwa wagombea wetu wa urais wanaona fahari kujibandika lebo.

Horace Kolimba anajiita "social democrat." Edwin Mtei anajiita "liberal democrat." Kwanza hizi si itikadi zao. Ni mikondo mbalimbali tu ya itikadi za kibepari. Wanaweza kuhoji. Ah! kwani kuafikiana na itikadi fulani ni dhambi? La hasha. Ni halali kabisa.

Lakini walipaswa wazijue na waweze kuzieleza na kuzitetea. Wajue historia yake na zinasimamia nini kwa sasa. Kwa maelezo yao wenyewe ambayo hatuna haja ya kuyarejea hapa, ni dhahiri kuwa hawazielewi. Kwa hiyo wanachofanya Horace Kolimba na Edwin Mtei ni usokwe mtu tu: kuiga hata jambo wasilolijua. Nukta.

Nafasi haitaruhusu kufafanua historia ya mikondo hiyo ya itikadi za kibepari. Inatosheleza tu kueleza kuwa social democrat ni itikadi iliyoibuka kulitaka tabaka la mapebari kulitupilia makombo kidogo tabaka la wafanyikazi katika nchi zenye viwanda katika nyakati ambapo matabaka hayo yalikuwa yakikinzana vikali.

Vyama vinavyojulikana kama "conservative" ni panya wa kuuma. Wakati vyama vinavyojulikana kama social democratic panya wa kupulizia, kulipunguzia makali ya kunyonywa tabaka la wafanyikazi.

Lakini vyote vinatumikia mfumo ule ule, tena kwa uaminifu mkubwa. Kwani ikibidi huungana kuwakandamiza wafanyikazi, hasa mfumo huo unapopata mtikisiko. Mara kadhaa huko Ujerumani vyama hivi vimeungana kwa nia tu ya kuzuia vyama vingine, hasa vyenye kuhoji mfumo wa ubepari, kuchukua madaraka.

Liberal Democrat ni itikadi ilyoibuka kama wasuluhishi au wasawazishaji wa 'ugomvi' baina ya conservative na social democrat. Wao huchukua msimamo wa kati. Hawa ni ndumiakuwili wa kwelikweli kama ilivyojidhihirisha huko Ujerumani. Hujiunga na kila anayekuwa madarakani.

Kolimba na Mtei walipaswa watuambie kama mazingira hayo yapo hapa kwetu. Kila mtu anajua kuwa hayapo. Kwa hiyo lebo walizojibandika zinadhihirisha ni kiasi gani walivyo mufilisi wa itikadi. Hawawezi kubuni itikadi zao ila kujibandikiza za wenzao.

Pengine wamenunuliwa au wanataka kujipendekeza kwa wakubwa. Lakini wakubwa hao hao ndiyo wetu ajae anatakiwa kulumbana nao kuhusu uwiano mbaya wa biashara duniani, uchafuzi wa mazingira, mgawanyo usio wa haki wa maarifa hasa ya sayansi na teknolojia, umaskini uliokithiri katika nchi zetu, udunishaji wa akina mama, mfumo usio wa haki wa maamuziki katika mashirika ya kimataifa hasa Umoja wa mataifa na kadhalika.

Licha ya itikadi za Kolimba na Mtei za kisokwe-mtu, mantiki yake ni 'kutia sumu kisimani kabla watu hawajachota maji.' Yaani wanataka watu wawahukumu kutokana na lebo walizojibandikiza na siyo kutokuwa na kauli na matendo yao. Kwa kuwa Kolimba na Mtei wamekuwapo tangu zamani tunajua kabisa kuwa kauli na matendo yao yanawasuta kuhusu hilo.

Kolimba amekuwa mwanachama na kiongozi wa siku nyingi wa chama kilichopata kujiita cha wakulima na wafanyikazi. Haijatokea hata mara moja chama hicho kikajibandika lebo ya social democrat. Je, huo ndio msimamo mpya wa chama chake? Kama siyo kwa nini tusimwite kinyonga kwa kujibandika rangi yoyote ili muradi tu inamnufaisha kwa wakati huo? Kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kukiuka itikadi ya chama chake? Au chama hicho sasa ni 'kapu kubwa' la zoa zoa ya kila itikadi?

MWELEKEO

Rais Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi. Kwa maana aliweza kubuni au kutengeneza mazingira yaliyowezesha mwelekeo wa taifa kubuniwa, kujadiliwa, kutekelezwa na kutathminiwa. Mwelekeo huo ulikuwa wa siasa ya ujamaa na kujitegemea.

Siyo wote tulioafikiana naye. Lakini tuliufahamu mwelekeo huo. Pia tulijua, ingawa si wote tulioafiki, mbinu na mikakati ya kulifikisha taifa huko. Yaani mali ya umma, ujamaa vijijini, elimu ya kujitegemea, huduma za jamii kama vile elimu na afya zilizogharimiwa na serikali na kadhalika.

CCM walibadili itikadi hiyo. Wala hawakuona haja ya kutafuta itikadi nyingine badala ya hiyo. Kwa sababu hiyo taifa hili sasa linashutumiwa kwa kutokuwa na mwelekeo. Kwa hiyo, kwangu mimi sifa ya kwanza kabisa ya rais lazima iwe kututangulia na sisi tukamfuata, au kutuonyesha njia na sisi tukaifuata. Yaani awe na uwezo wa kubuni na kusimamia usanifu wa mwelekeo wa nchi.

Katika wagombea wote waliohojiwa ni Joseph Sinde Warioba tu aliyetamka neno mwelekeo. Anasema ana mawazo kuhusu mwelekeo wetu katika miaka ijayo. Kwake yeye mwelekeo huo ni umoja, amani na utulivu. Haya ni maneno mazuri sana masikioni lakini yasiyokuwa na maana yoyote kichwani.

Kwanza, Umoja, amani na utulivu haviwezi kuwa mwelekeo wa nchi. Hizo ni hali. Siyo lengo bali ni hali inayoruhusu malengo kutimizwa. Warioba na wagombea wengine wote wanapaswa watuambie, je kukisha kuwa na amani, umoja na utulivu kutafuata nini? Ni taifa lenye mahusiano gani ya kijamii litakalojengwa?

Kazi / Masomo mema, Emmanuel Muganda